Listen

Description

*KITU CHA KUKUVUSHA ULIPOKWAMA KIKO NYUMBANI MWAKO*
_STRETCH !_
By Luphurise Mawere

*2 Wafalme 4: 1-7*
_1 Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha BWANA; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa._

_2 Elisha akamwambia, Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta._

_3 Akasema, Nenda, ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache._

_4 Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge._

_5 Basi akamwacha, akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, na yeye akamimina._

_6 Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, Hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma._

_7 Ndipo akaja akamwambia yule mtu wa Mungu. Naye akasema, Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako._

Unaposoma mistari hiyo hapo juu tunamuona Mwanamke mjane ambaye alikuwa na madeni.
Kipindi hicho kulikuwa na utaratibu wa masikini na wadaiwa kuuza watoto wao kuwa watumwa ili walipie madeni yao.
Mwanamke huyu alikuwa kwenye wakati mgumu sana alikuwa kwenye *financial crisis*.
Kama ilivyo wengi wetu akamlilia mtumishi wa Mungu, Nabii Elisha
Mwanamke huyu alikimbilia sehemu sahihi.
Cha ajabu mtumishi wa Mungu Nabii Elisha anamuuliza huyu mjane, Nikufanyie nini? Au Nikusaidie nini?
Hebu jiweke kwenye viatu vya huyu Mwanamke, uko kwenye changamoto ngumu unamlilia mtumishi wa Mungu unayemwamini anakuuliza Nikusaidieje?
Lakini swali la pili aliloulizwa na mtumishi wa Mungu Elisha linafunua siri kubwa sana, anamuuliza tena UNA KITU GANI NYUMBANI KWAKO?
Yule mwanamke mjane anajibu sina kitu nyumbani ila chupa ya mafuta, ina maana aliona hiyo chupa ya mafuta sio kitu.
Lakini tunaona kila ambacho huyu mjane aliona sio kitu ndicho ambacho Mungu alikitumia kumtoa mjane huyu kwenye shimo la madeni na kunusuru watoto wake na utumwa na kumfanya huyu mama kuwa msambazaji wa mafuta.
Mungu anazungumza na wewe mpendwa wangu unayelia, unayesema mambo yako ni magumu, gari lako linataka kuuzwa, viwanja vyako na nyumba yako vinataka kuuzwa,
Umekata tamaa kwasababu unafikiri huna kitu
Mungu anakuuliza asubuhi ya leo UNA KITU GANI NYUMBANI KWAKO?
Usiseme sina kitu
Hebu kagua nyumba yako
Hebu jikague
Labda chupa yako ni hiyo bustani, au huo ujuzi wa kusuka, kufuma au huko kufundisha, labda ni huko kuimba, hichohicho unachofikiri sio kitu Mungu atakitumia kukukwamua hapo ulipo.
_Efeso 3: 20 Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu;_
Mpendwa unachotakiwa kufanya ni *ku- STRETCH*, fanya zaidi, ongeza Imani, mruhusu Mungu atumie hicho unachoona sio kitu kukukwamua na kukuvusha hapo ulipo.
*STRETCH !*

Maelekezo zaidi;
*+255 754 934693*