Listen

Description

_*Yohana 16: 33* Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu._

_*Ayubu 1: 22* Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu._
(Soma Ayubu yote mlango 1 na wa 2)

Bwana Yesu hatukuahidi kwamba tutaishi tu kwa furaha siku zote
Hatukuahidiwa kwamba kila siku itakuwa birthday, wedding anniversary au party
Nakumbuka nikiwa chuoni kuna wadada walikatiwa jina _"Everyday is holiday"_maana wao walikuwa kuanzia Jumatatu hadi Jumapili walikuwa busy kwenye starehe wakasahau kabisa kwamba walikuwa pale kwa lengo la kusoma
Yesu hakutuambia kwamba everyday is holiday, katika maneno yake anasema ulimwenguni mnayo dhiki, tutapata shida na tutakutana na magumu
Je ulishawahi kukutana na mambo magumu?
Ulishawahi kupitia mapito?
Au ndio uko kwenye mapito sasa na magumu?
Yesu anatuambia TUJIPE MOYO tafsiri za Biblia za Kiingereza zinasema _"be of a good cheer"_ na _"cheer up"_ yaani furahi.
Hapo najua utashangaa na kujiuliza nifurahi?
Kwanini ufurahi wakati ndoa yako imekufa, wakati umefukuzwa au kupunguzwa kazi, wakati umeondokewa na mpendwa wako, wakati biashara yako imekufa, wakati huna ada ya shule, wakati mchumba amekuacha kwenye mataa?
Bwana Yesu anatuambia tufurahi kwasababu yeye Mfalme wa Wafalme AMEUSHINDA ulimwengu na kama yeye ameshinda na wewe pia umeshinda, Halleluya!
_1 Yohana 5: 4 Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu._
Utashinda changamoto na mapito magumu ya ulimwengu huu kwasababu umezaliwa na Mungu
Ayubu alikuwa mwanadamu kama mimi na wewe na alipitia mapito mazito
Katika Coaching Sessions na ushauri wa kiroho ninaofanya kwa watu nimekutana na watu wenye mapito magumu lakini sijakutana na hata mmoja anayemfikia Ayubu
Ukisoma Ayubu mlango wa 1 wote utaona namna alivyopoteza watoto 10, mali zote, afya ikaterereka na mke wake badala ya kumtia moyo akawa kinyume naye
Ayubu alitambua kwamba pamoja na mapito yote aliyopitia AMEUSHINDA ulimwengu hivyo alijipa moyo na kuwa na mtazamo chanya katikati ya mapito magumu

*Ufanyeje ili uweze kuwa na Mtazamo Chanya ukipitishwa kwenye magumu?*
_1 Yohana 5: 5 Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu?_

Mpendwa ninajua sio rahisi kuwa na mtazamo chanya unapopitia magumu
Kitu kitakachokusaidia kuwa na mtazamo chanya wakati unapitia magumu ni kuwa na mahusiano mazuri na Mungu wako. Kwa kumpa Yesu maisha yako kwa kumaanisha ili kumwacha Yesu awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako. Umruhusu aingie ndani yako nawe uwe ndani yake
Unapokuwa umempa Yesu maisha yako kwa kumaanisha ya kuokoka toka moyoni ndipo utakapokuwa na Ujariri wa kusema maneno aliyoyasema Ayubu mlango _1: 21 akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; BWANA alitoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na libarikiwe._
Hata kama umepitia magumu kiasi gani
Unapokuwa umembeba Yesu maishani mwako utatambua kwamba vyote ulivyonavyo ni mali ya Mungu wewe ni wakili tu
Mke, mume, watoto, kazi, biashara, mali, elimu, ndoa, huduma ulizonazo sio vya kwako
Ikitokea vinaondoka utajikuta tu unanyoosha mikono juu kama Ayubu hata kama unalia na maumivu mengi ukimwambia Mungu, Baba asante hata hatika haya maana najua utanishindia
Kwahiyo mpendwa wangu hebu JIPE MOYO, hebu furahi, tazama ukuu wa Mungu, ukiendelea kulia sana na kusononeka sana kwa hivyo vitu kuondoka vinageuka kuwa _"mungu"_ kwako, vinachukua nafasi ya Mungu, ina maana unaviabudu
Mpendwa Mungu wetu ni Mungu mwenye wivu, yeye ndio anatakiwa kuchukua nafasi ya kwanza maishani mwetu
Amua leo kuinuka, anua hilo turubali, maliza huo msiba, maliza hicho kilio mpendwa,
JIPE MOYO, Furahi, cheer up
Wewe ni MSHINDI
_Kama unahitaji msaada namna ya kuvuka kwenye mapito unayopitia tuwasiliane
Mungu anakupenda sana!