Listen

Description

USIFICHE TALANTA YAKO
_By Luphurise Mawere_

Mathayo 25: 14-18
_Mathayo 5: 15 Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani._

Habari tuliyosoma kwenye Kitabu cha Mathayo 25: 14-18 inafananishwa na maisha yetu hapa duniani.
Mungu amewekeza ndani yetu talanta, yaani ameweka karama, vipawa, ujuzi na maarifa.
Kila mtu amepewa kadri uwezo wake, na Mungu anatutegemea kile alichowekeza ndani yetu kitumike hata kama unakiona ni kidogo kuliko wengine.
Tuepuke kabisa kuwa kama mtu huyu aliyepewa talanta moja yeye badala ya kuzalisha akaifukia chini.
Watu wengi wanafukia uwezo yaani potential Mungu alizoweka ndani yao kwasababu wanafikiri ni ndogo au haifai.
Mpendwa inabidi utambue kwamba hicho kitu ulichonacho kuna mtu anakihitaji ili aweze kuvuka kwahiyo ukikificha kuna mtu atakwama.
Neno la Mungu linasema katika _Warumi 8: 19 Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu._

Kitu kilicho ndani yako kinaweza kuonekana kidogo au hakina maana machoni pa wengi, lakini mbele za Mungu ni muhimu na kinahitajika sana ili kuleta mabadiliko kwenye ufalme.
Inawezekana wewe talanta yako ni kutia moyo tu, ukamtia moyo mtu mmoja ambaye amekata tamaa na anatamani kujiua akapata tumaini na baadae kusimama katika kusudi lake.
Huduma ninayoiongoza ya Soaring Women International tulianza kufanya Summit za Wanawake mwaka 2017, nilianza kwa woga mkubwa mno sikujua kama italeta badiliko kwenye maisha ya watu. Mwaka 2019 mwanamke mmoja alishuhudia namna ambavyo alitaka kujiua kutokana na changamoto alizokuwa anazipitia lakini akasikia tangazo la Summit ya 2017 na alipokuja Mungu alimuhudumia sana ile hali ya kutaka kujiua ikaondoka hadi sasa yuko hai. Ina maana ningeficha hiyo talanta huyo mama angeweza kupoteza maisha.

Kuna mama mmoja anaitwa Mama Kigelegele, huyu mama anakodishwa kwenye shughuli mbalimbali kupiga kigelegele. Na pia anakitumia kama njia ya uinjilisti.
Kikawaida kigelegele unaweza kuona hakina maana na sio kitu kinachoweza kumsaidia mtu chochote. Mama huyu alikataa kukificha kigelegele chake na ame-STRETCH kigelegele chake kimekuwa ndio chanzo chake kikubwa cha mapato.
Kupitia kigelegele ameweza kusomesha watoto wake hadi chuo kikuu na kufanya vitu vingi vya maendeleo.
Amehojiwa na vyombo vikubwa vya habari kama BBC n.k
Ameweza kuingia maeneo ambayo hakutegemea kwa kigelegele tu.

Leo nakupa changamoto, jichunguze, Talanta yako ni nini?
Una karama, kipawa, ujuzi gani?
Je unavitumia?
Kitu gani kinakuzuia kuvitumia?
Wengi hawatumii talanta zao kwasababu wanajilinganisha na wengine
Mpendwa usifanye hilo kosa kumbuka Mungu amempa kila mtu kwa *kadri ya uwezo wake*.
Jukumu lako ni kutambua yako na kuifanyia kazi, usiweke taa yako chini ya pishi.
Ulichonacho ni cha thamani sana mbele za Mungu
Unamkumbuka Daudi?
Alikuwa tu mchunga kondoo.
Ila alitambua kuwa japo yeye ni kijana mdogo tena mchunga kondoo ndani yake Mungu amewekeza uwezo wa kumpiga Goliathi Mfilisti aliyekuwa tishio kwa wana wa Israeli.
Daudi ali-STRETCH na alifanikiwa kumpiga Goliathi kwa jiwe moja tu akafa.

Ndugu yangu STRETCH
Fanya zaidi
Panua mahali pa hema yako
Usifiche talanta yako
Usiweke taa yako chini ya pishi
Usiangalie uwezo wa wengine
Enenda kwa uwezo wako huo
Hichohicho kinachoonekana kidogo , kinyonge au kidhaifu ukisimama kwa Imani Mungu atakitumia kuleta mabadiliko makubwa kwenye ufalme wake.
Usiseme sijasoma
Usisema siwezi kuongea
Usiseme hakuna anayekujua

Unaweza kwakuwa aliye upande wako ni mkuu
Kuwa hodari na moyo wa ushujaa

Mawasiliano
*+255 754 934693*