Baada ya kuwa na tofauti kwa wakongwe wa muziki wa Bongo Fleva kutokea Tanzania, kati ya msanii Prof Jay na mtayarishaji P Funk, inaonekana kwa sasa wawili hao wameweka pembeni tofauti zao na sasa hivi ni kazi tu.
Prof Jay ambae pia ni mbunge wa jimbo la Mikumi mkoani Morogoro, ameposti picha kupitia account zake za Instagram na Twitter akiwa na mtayarishaji huyo ndani ya studio yake ya Mwanalizombe iliyopo Mikumi Morogoro.
Baada ya kuposti picha hiyo, Prof Jay akaandika hivii,
"Ni baraka juu ya baraka Mwanalizombe studio inazidi kupasua anga, "Bomb Bomb fire, na leo tumebahatika kutembelewa magomvi wawili Mwana Fa na P Funk majani, Yaliyopita si ndwele tumeamua kuganga yajayo, Tumerudi kufanya kazi pamoja tukiwa imara zaidi, Yajayo yanafurahisha eeeeeh! Mwenyezi Mungu atusaidie"
Mashabiki na baadhi ya mastaa mbalimbali walionekana kufurahishwa baada ya kuona wawili hao kuungana pamoja, huku wengine wakisema hiyo ni picha bora ya mwezi Julai.
Ukaribu wao uliingia tofauti baada ya mtayarishaji P Funk kupokea kiasi cha milioni 100 za kitanzania za haki miliki za wimbo alioutengeneza ambao ulitumiwa na wasanii wa Uganda, ambapo COSOTA walidai kwamba pesa hizo alilipwa Prof Jay.