“Msiwahukumu wengine, msije nanyi mkahukumiwa na Mungu; 2kwa maana jinsi mnavyowahukumu wengine, ndivyo nanyi mtakavyohukumiwa; na kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho Mungu atakachotumia kwenu. 3Kwa nini wakiona kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako? 4Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako,’ wakati wewe mwenyewe unayo boriti jichoni mwako? 5Mnafiki wewe! Ondoa kwanza boriti iliyomo jichoni mwako na hapo ndipo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilichomo jichoni mwa ndugu yako.
6“Msiwape mbwa vitu vitakatifu wasije wakageuka na kuwararua nyinyi; wala msiwatupie nguruwe lulu zenu wasije wakazikanyaga.
7“Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata; bisheni mlango, nanyi mtafunguliwa. 8Maana, yeyote aombaye hupewa, atafutaye hupata, na abishaye mlango hufunguliwa. 9Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba mkate, atampa jiwe? 10Au je, akimwomba samaki, atampa nyoka? 11Kama basi nyinyi, ingawa ni waovu, mwajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika Baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi: Atawapa mema wale wanaomwomba.
12“Yote mnayotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo. Hii ndiyo maana ya sheria ya Mose na mafundisho ya manabii.
13“Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba. Kwa maana njia inayoongoza kwenye maangamizi ni pana, na mlango wa kuingilia humo ni mpana; waendao njia hiyo ni wengi. 14Lakini njia inayoongoza kwenye uhai ni nyembamba, na mlango wa kuingilia humo ni mwembamba; ni watu wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo.
Mti hujulikana kwa matunda yake
15“Jihadharini na manabii wa uongo. Wao huja kwenu wakionekana kama kondoo kwa nje, lakini kwa ndani ni mbwamwitu wakali. 16Mtawatambua kwa matendo yao. Je, watu huchuma zabibu katika miti ya miiba, au tini katika mbigili? La! 17Basi, mti mzuri huzaa matunda mazuri, na mti mbaya huzaa matunda mabaya. 18Mti mzuri hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. 19Kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni. 20Kwa hiyo, mtawatambua kwa matendo yao.