Yesu anaamuru dhoruba itulie
23Yesu alipanda mashua, na wanafunzi wake wakaenda pamoja naye. 24Mara, dhoruba kali ikatokea ziwani, hata mawimbi yakaanza kuifunika mashua. Yesu lakini alikuwa amelala usingizi. 25Wanafunzi wakamwendea, wakamwamsha wakisema, “Bwana, tuokoe, tunaangamia!” 26Yesu akawaambia, “Enyi watu wenye imani haba; mbona mnaogopa?” Basi, akainuka, akaukemea upepo na lile ziwa; kukawa shwari kabisa. 27Watu wakashangaa, wakasema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata pepo na bahari vinamtii!”
Yesu anaponya watu wawili wenye pepo
28Yesu alifika katika nchi ya Wagadara, ngambo ya ziwa, na huko watu wawili waliopagawa na pepo wakakutana naye wakitokea makaburini. Watu hawa walikuwa wenye kutisha mno, hata hakuna mtu aliyethubutu kupita njia hiyo. 29Nao wakaanza kupiga kelele, “Una shauri gani nasi, wewe Mwana wa Mungu? Je, umekuja kututesa kabla ya wakati wake?”
30Karibu na mahali hapo kulikuwa na nguruwe wengi wakichungwa. 31Basi, hao pepo wakamsihi, “Ikiwa utatutoa, basi uturuhusu tuwaingie nguruwe wale.” 32Yesu akawaambia, “Haya, nendeni.” Hapo wakawatoka watu hao, wakawaingia nguruwe. Kundi lote la nguruwe likaporomoka kwenye ule mteremko mkali, likatumbukia ziwani; nguruwe wote wakafa majini.
33Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakaenda mjini. Huko walitoa habari zote na mambo yaliyowapata wale watu waliokuwa wamepagawa. 34Basi, watu wote katika mji ule walitoka, wakamwendea Yesu; na walipomwona, wakamsihi aondoke katika nchi yao.