Listen

Description

Habari Mwanamafanikio?

Karibu usikilize kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambacho kina mambo makubwa na muhimu kama ifuatavyo;

Kwenye somo la juma utajifunza umuhimu wa Kuandika vitu ili uweze kufikiri vizuri na kuweza kuvikamilisha. Unapofikiria tu vitu huvipi msisitizo mkubwa kama ukiviandika chini. Hivyo unapaswa kujijengea utamaduni wa kuyaandika malengo yako kila siku, kuandika mipango yako ya siku, kuandika yale uliyojifunza na kuandika tathmini zako binafsi. Sikiliza kipindi kujifunza hilo kwa kina.

Kwenye kitabu cha wiki utapata uchambuzi wa kitabu Dedicated: The Case for Commitment in an Age of Infinite Browsing kilichoandikwa na Pete Davis. Kitabu kinaelezea tamaduni mbili zinazokinzana, wa kwanza ni wa kuperuzi kusiko na ukomo, yaani kubaki na machaguo mengi bila ya kujitoa kwenye kitu kimoja. Utamaduni wa pili ni wa kuchagua kitu kimoja, kujitoa kweli kwenye kitu hicho na kupuuza vitu vingine. Kwenye zama hizi wengi wametekwa na utamaduni wa kuperuzi ndiyo maana wanashindwa kufanya makubwa. Pete ametushirikisha jinsi tunavyoweza kujijengea utamaduni wa kujitoa ili kuweza kufanya makubwa.

Muhimu zaidi ni kitabu hiki ndiyo kinachotupa mwongozo na mwelekeo mkubwa wa KISIMA CHA MAARIFA kwa sababu tunakwenda kujenga jamii ya tofauti kwenye KISIMA, jamii inayochagua na kujitoa kwenye kitu ili kufika ubobezi wa hali ya juu na kuleta mabadiliko makubwa. Vitu muhimu kabisa kwa ajili ya KISIMA CHA MAARIFA kutoka kwenye kitabu hiki ni kila mtu kujua KUSUDI lake, kuwa na NDOTO kubwa, kuwa kwenye KLABU na kuishi kwa misingi iliyopo kwenye KISIMA. Sikiliza kipindi na pia soma uchambuzi wa kitabu hicho ili kujifunza kwa kina zaidi.

Kwenye mahojiano na mwanamafanikio tumepata nafasi ya kuongea na mwanamafanikio mwenzetu Selemani Mbwambo ambaye anatushirikisha safari yake ya mafanikio. Selemani anatushirikisha jinsi alivyoacha ajira ya ualimu na kuanza biashara ya vifaa vya baiskeli kwa mtaji wa shilingi laki tano. Mpaka sasa biashara imekuwa na ameweza kutanuka zaidi na kuweza kuwa na biashara ya vifaa vya ujenzi (hardware). Kwenye mahojiano haya utajifunza mengi kupitia safari ya Selemani ambayo unaweza kuyatumia kwenye safari yako ya mafanikio.

Mwisho kuna mjadala wa wanamafanikio wote, ambao wametoa michango, kushirikisha waliyojifunza na kuuliza maswali mbalimbali. Kupitia mjadala huo yapo mengi pia ya kujifunza.

Karibu usikilize kipindi hiki, ujifunze na kwenda kuchukua hatua ili kuweza kufanya makubwa zaidi.

Usisahau kwamba KISIMA CHA MAARIFA ni jeshi, tunakwenda kuweka juhudi kubwa kujenga jamii ya tofauti ambayo itakuwa nuru kwa jamii kubwa inayotuzunguka. Mchango wako ni muhimu sana kwenye safari hii. Karibu sana twende pamoja.

Kocha.



This is a public episode. If you would like to discuss this with other subscribers or get access to bonus episodes, visit mafanikio.substack.com