Habari Mwanamafanikio?
Kwenye KISIMA CHA MAARIFA, tupo kwenye muongo (2020 - 2030) wa kufanya makubwa.
Katika muongo huu kila mmoja wetu anapambana kufikia uhuru wa kifedha, ambapo ni kuweza kuwa na njia za kuingiza kipato kisichotegemea uwepo wa moja kwa moja (passive income) pamoja na kuwa na uwekezaji mkubwa unaokua thamani na kuzalisha faida inayoweza kukidhi gharama za kuendesha maisha.
Katika kufanyia kazi lengo hilo, tuna kitabu ambacho ndiyo mwongozo wetu kwa kipindi hiki chote. Kitabu hicho ni BILLIONAIRE IN TRAINING ambacho kimeandikwa na Bradley Sugars.
Kitabu hiki kimeelezea njia tatu za kufika kwenye utajiri na uhuru wa kifedha ambazo ni kama ifuatavyo;
Moja ni kuingiza kipato kisichotegemea uwepo wako (passive income cashflow).
Mbili ni kufanya uwekezaji kwenye mali kama ardhi na majengo (real estate).
Na tatu ni kufanya uwekezaji kwenye masoko ya mitaji kama hisa, hatifungani na vipande (paper assets).
Njia kubwa ya kufanyia kazi ili kuweza kutengeneza utajiri kwenye njia hizo tatu ni kuwa na biashara ambayo inajiendesha yenyewe kwa mfumo, ambayo haitegemei uwepo wako moja kwa moja.
Na hapo ndipo kitabu hiki kinakwenda kuwa mwongozo mkubwa kwetu, kwani ndiyo tunakitumia kujenga na kuendesha biashara zinazotupa uhuru mkubwa.
Na haiishii hapo tu, bali tunajifunza kununua, kukuza na kuuza biashara ili kuweza kutengeneza faida kubwa kupitia mfumo tunaokuwa tumeujenga.
Karibu sana kwenye mjadala wa kitabu hicho, ujifunze jinsi ya kufanyia kazi yale yanayopatikana kwenye kitabu ili kuweza kulifikia lengo la uhuru wa kifedha kwa uhalisia.
Kwa kuwa kitabu hiki ndiyo mwongozo, tutaendelea kujifunza kwa kina na kufanyia kazi kila kinachofundishwa kwenye kitabu hicho bila ya kuacha hata kimoja.
Mjadala huu umesheheni mengi sana ya kufanyia kazi kwa popote ulipo sasa na uweze kupiga hatua kubwa zaidi.
Karibu usikilize, ujifunze na uchukue hatua ili kuyafikia malengo yako ya muongo.
Kocha.