Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza Aidan Eyakuze amesema kwamba ni wajibu wa wananchi kuhakikisha kwamba Serikali yao inafanya mambo kwa uwazi ili kuchochea uwajibikaji hali inayoweza kuchangia kuboresha hali zao za maisha kiuchumi na kijamii.
Eyakuze, ambaye shirika lake linafanya kazi zake nchini Tanzania, Uganda na Kenya kuchochea uwazi na uwajibikaji serikalini, alitoa kauli hiyo wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika ofisini kwake hapo Julai 8, 2022.
“Hii Serikali inakutumikia wewe, wewe si mtumishi wa Serikali,” alisema Eyakuze, ambaye pia ni Mwenyekiti-mwenza wa Open Government Partnership, mpango wa kidunia unaopigania uwazi, ushirikishwaji wa wananchi na uwajibikaji serikalini. “Wewe ndiyo mwajiri wa hiyo Serikali.”